Alhamisi asubuhi tarehe 21.09.2023
2 Wakorintho 11:23-30
23 Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.
24 Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
25 Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.
28 Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.
29 Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?
30 Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.
Mungu hujishughulisha na maisha yetu;
Kazi ya kuhubiri Injili kwa Mtume Paulo haikuwa nyepesi. Asubuhi hii tunamsoma Paulo alivyopitia magumu mengi katika kazi hiyo. Anaandika alivyopigwa na kufungwa, akijiona kupita katikati ya mauti. Alipigwa mawe, bakora, alivunjikiwa jahazi! Zilikuwepo hatari za kusafiri majini, wanyang'anyi, hatari za baharini na jangwani, kukesha mara nyingi, njaa, kiu na baridi kali. Hakika kazi yake haikuwa rahisi.
Pamoja na Paulo kupitia magumu yote hayo, bado aliitenda kazi ya Mungu kwa ujasiri na uaminifu. Naweza kusema Mungu alijishughulisha na kazi ya Paulo kuhubiri Injili. Kama ambavyo Mungu hakumuacha Paulo, hajatuacha nasi hata leo. Hujishughulisha na maisha yetu. Hivyo tuishi katika yeye, sasa na siku zote. Amina.
Heri Buberwa