Jumatatu asubuhi tarehe 22.08.2022
Luka 4:38-43
[38]Akatoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake.
[39]Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia.
[40]Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya.
[41]Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo.
[42]Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao.
[43]Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa.
Tutumie vizuri nafasi tuliyopewa;
Bwana Asifiwe;
Yesu aliingia kwenye nyumba ya Simoni akamkuta mkwe wa Simoni aliyekuwa na homa. Yesu alipoombwa akamponya. Na wagonjwa wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali waliletwa kwa Yesu wakaponywa, wakiwemo waliotokwa na pepo.
Hata kulipokucha watu waliendelea kumfuata wakimtaka asiondoke kwao. Lakini yeye akawaambia ilimpasa kuondoka akaendelee kuhubiri, kufundisha na kuponya.
Tunaona Yesu alipoombwa kumponya mkwe wa Simoni alimponya homa aliyokuwa nayo. Wagonjwa walipoletwa kwake waliponywa maradhi mbalimbali. Tunachokiona watu walitumia fursa ya Yesu kuwepo wakaponywa. Hawakuacha apite tu. Kumbe na sisi tuitumie fursa ya Imani yetu katika Kristo, tukiomba neema ya Mungu katika maisha yetu ili kufanikiwa, na hatimaye tuurithi uzima wa milele.
Tutumie vizuri nafasi tuliyopewa.
Tunakutakia wiki njema.