Date: 
22-09-2022
Reading: 
2 Samweli 24:18-23

Alhamisi asubuhi tarehe 22.09.2022

2 Samweli 24:18-23

18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, Haya! Kwea wewe, ukamwinulie Bwana madhabahu penye kiwanja cha Arauna, Myebusi.

19 Basi Daudi akakwea sawasawa na neno la Gadi, kama Bwana alivyoamuru.

20 Huyo Arauna akatazama, akamwona mfalme na watumishi wake wakimjia; Arauna akatoka, akasujudu mbele ya mfalme kifulifuli hata nchi.

21 Arauna akasema, Bwana wangu mfalme amemjia mtumwa wake kwa kusudi gani? Naye Daudi akasema, Makusudi ninunue kwako kiwanja hiki, ili nimjengee Bwana madhabahu, ili kwamba tauni ipate kuzuiliwa katika watu.

22 Arauna akamwambia Daudi, Bwana wangu mfalme na akitwae, akatolee yaliyo mema machoni pake; tazama, ng'ombe hawa kwa sadaka ya kuteketezwa, tena vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng'ombe, viko kwa kuni,

23 vitu hivi vyote, Ee mfalme, mimi Arauna nakupa wewe mfalme. Kisha Arauna akamwambia mfalme, Bwana, Mungu wako, na akukubali.

Uwakili wetu kwa Mungu;

Israeli walimchukiza Mungu, mfalme Daudi akaambiwa achague adhabu kati ya;

-miaka 7 ya njaa

-kukimbia mbele ya adui zake huku akifukuzwa

-Tauni ipige kwa siku tatu katika nchi

Daudi akachagua kuangukia mikononi mwa Bwana na sio wanadamu, hivyo walikufa watu wengi zaidi ya elfu sabini kwa tauni.

Ndipo somo la leo asubuhi sasa, nabii Gadi anatumwa na Mungu kumjia Daudi akimuelekeza akamjengee Bwana madhabahu na kutoa sadaka, kwenye kiwanja cha mtu aliyeitwa Arauna. Arauna alikuwa tayari kutoa kiwanja bure, lakini Daudi alikataa, akakitwaa kiwanja kwa fedha, siyo bure.

Tunajifunza nini?

1.Mtolee Bwana kwa moyo

Arauna alikuwa tayari kutoa kiwanja kwa ajili ya kumwabudu Bwana. Hakutaka fedha yoyote! Bila shaka huu ni moyo wa ibada, uliopenda kuona Mungu akiabudiwa. Hivyo kumtolea Mungu hakuona shida. Mtolee Mungu kwa moyo.

2. Fanya kazi kwa bidii.

Pamoja na kupewa kiwanja bure, Daudi hakuwa tayari, alitoa fedha ili kumlipa Arauna ampe kiwanja. Hakutaka kiwanja cha bure. Naweza kusema tafsiri yake ni kuwa mali inapatikana kwa kufanya kazi. Daudi alitoa fedha. Tafsiri ya fedha ni nguvu, muda, mali na utayari wa kutumika. Fanya kazi kwa bidii upate mali ya halali, tayari kumtolea Bwana.

Alhamisi njema.