Date:
01-05-2023
Reading:
Wagalalita 1:6-9
Hii ni Pasaka
Jumatatu asubuhi tarehe 01.05.2023
Wagalatia 1:6-9
6 Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.
7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.
8 Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.
9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.
Maisha mapya ndani ya Yesu;
Paulo aliandika waraka huu baada ya safari yake ya kwanza ya kitume na kuanzisha makanisa sehemu ya Kusini mkoani Galatia. Sehemu hiyo sasa ni Uturuki. Baada ya Paulo kutoka Galatia, baadhi ya Wakristo wa Kiyahudi walifika huko wakafundisha kwamba ili wakristo wakamilike katika wokovu hawana budi kufuata mila, desturi na sheria za dini ya Kiyahudi.
Wakristo hawa wa Kiyahudi walidai kuwa ili mtu apate kuokolewa anapaswa kutahiriwa na kuishika torati ya Musa, wakisema imani na ubatizo katika Yesu havitoshi! Walisema Paulo siyo mtume, bali mwanafunzi tu wa Petro na Yakobo. Wagalatia waliyaamini madai haya, madai ambayo ndiyo ilikuwa ajenda ya Mkutano wa Kanisa hapo Yerusalemu (Mdo 15)
Paulo aliandika waraka huu kukanusha madai haya ya kikundi cha Wayahudi. Aliyakemea akisema ni uòvu katika waraka huu.
Ndipo kwa sehemu katika somo la asubuhi hii Paulo anawashangaa Wagalatia kumwacha Yesu aliyewaita na kufuata Injili ya namna nyingine. Paulo anakazia kuwa Injili ya Yesu Kristo ndiyo Injili ya kweli iokoayo, na yeyote ahubiriye kinyume na hiyo alaaniwe.
Nasi asubuhi ya leo tunakumbushwa kuwa Injili ya Yesu Kristo ndiyo iliyo ya kweli kama tulivyoipokea. Tuendelee kumwamini Yesu kwa njia ya neno lake, na siyo Injili nyinginezo za kutupoteza. Tukimshika Yesu Kristo, tukadumu katika neno lake, maisha yetu yanakuwa mapya siku zote. Amina.
Mei Mosi njema
Heri Buberwa