Hii ni noeli
Ijumaa asubuhi tarehe 27.12.2024
2 Mambo ya Nyakati 24:18-22
18 Wakaiacha nyumba ya Bwana, Mungu wa baba zao; wakatumikia maashera na sanamu; ghadhabu ikawajia Yuda na Yerusalemu kwa sababu ya hiyo hatia yao.
19 Hata hivyo akawapelekea manabii, ili kuwarudisha kwa Bwana; nao wakawashuhudia; lakini hawakukubali kuwasikiliza.
20 Na roho ya Mungu ikamjia Zekaria, mwana wa Yehoyada, kuhani; naye akasimama juu ya watu, akawaambia, Mungu asema hivi, Kwani ninyi kuzihalifu amri za Bwana, hata msiweze kufanikiwa? Kwa kuwa mmemwacha Bwana, yeye naye amewaacha ninyi.
21 Basi, wakafanya shauri juu yake, wakampiga kwa mawe kwa amri ya mfalme katika ua wa nyumba ya Bwana.
22 Basi hivyo mfalme Yoashi hakuukumbuka wema, ambao Yehoyada, baba yake, alimfanyia, bali alimwua mwanawe. Naye alipokufa, alisema, Bwana na ayaangalie haya, akayatakie kisasi.
Uwe shahidi mwaminifu wa Kristo hata kufa;
Yoashi alikuwa kijana aliyemtumaini Mungu. Kwa mwaka mmoja tayari alinusurika kifo pale bibi yake Athalia mwovu alipowatupa watoto wake. Alikulia hekaluni na walezi wake Yehoyada (kuhani) na Yehosheba waliomwiba katikati ya kaka zake waliouawa. Kama John Wesley ambaye alikosakosa kuungua kwenye nyumba iliyokuwa ikiungua akiwa mtoto, ni kama Yoashi naye aliokolewa toka motoni. Kwa miaka saba tu akatawazwa mfalme.
Alianza uongozi wake vizuri akilitengemaza hekalu lililopoteza hadhi yake wakati wa bibi yake Athalia akitawala nchi. Alihakikisha kwa makuhani kurejesha nchi katika njia sahihi, maana hapo kabla hawakuweza kufanya kazi zao kwa ukamilifu.
Baada ya kupata mazingira ya Yoashi kutawala; somo la leo linaanzia hapa;
Baada ya kuhani Yehoyada kufariki, viongozi wa Yuda walimjaribu Yoshua, wakimwacha Bwana, wakaanza kuabudu miungu (24:18). Yoashi alikataa sauti za kinabii zilizomuita kumrudia Bwana. Mwishowe alimuua kijana (au huenda mjukuu) wa kuhani Yehoyada, mpwa wake aliyempinga.
Jeshi dogo la waashuru liliivamia Yerusalemu. Joashi aliondoa hazina hekaluni na kumtumia mfalme wa Ashuru (2Fal 12:18). Ilichukua kama mwaka mmoja tu, baadaye maofisa wa Yuda waliuawa, na kumuacha Yoashi akiwa majeruhi. Watumishi wake wawili walimfitini wakamuua kitandani kwake, akafariki akiwa na miaka 47. Hakupewa heshima ya kuzika katikati wa wafalme wa Yerusalemu. Alikuwa kijana mzuri, aliyeondoka vibaya.
Habari hii ya Yoashi inatufundisha kuwa "upendeleo wa kiroho, huhitaji uhalisia wa kiroho, vinginevyo itakuwa kusumbuka kiroho". Tunaweza kuimulika historia ya Yoashi kupata uhusiano na maisha yetu kama ifuatavyo;
1.Yoashi alipewa upendeleo kiroho, kama sisi;
Yoashi alikua katika kaisha ya kawaida, pia ni dhahiri kuwa mkono wa Bwana ulikuwa upande wake. Kwa nini kaka zake walichinjwa na kufa yeye akabaki? Tena akiwa na mwaka mmoja? Kwa aliokolewa asife na Yehoyada kuhani na Yehosheba waliomkuza katika njia ya Bwana? Wote waliomsaidia asife hakuna aliyekuwa ndugu yake wa karibu! Ndiyo maana nashawishika kusema kuwa Bwana alikuwa upande wake.
Nasi tuko hivyo hivyo. Hii ni hasa kwetu tuliokulia katika malezi ya Kikristo. Wazazi wetu walitulea wakituelekeza jinzi ya kumfuata Yesu, kwa kuwa na imani, kusali, kusoma neno la Mungu na kutoa sadaka. Huu ni upendeleo kiroho toka Mungu kwetu sisi.
Hapo ulipo, tafakari kiwango cha upendeleo uliopewa, kwamba uko katika nchi ambayo unafanya ibada kwa uhuru. Kuna mahali hawawezi kusali! Pengine wakrito hawapo! Tuko kwenye nchi ambayo unaweza kupata neno la Mungu nyumbani, Kanisani, Jumuiya, Redioni, kwenye Televisheni, gazetini, mitandao ya kijamii, mikutano ya injili, semina, ushirika (fellowship), matangazo n.k Huu ni upendeleo kwangu, kwako na kwetu sote.
Tunaishi katika utamaduni wa kulaumu wazazi kwa kutokuwa wakamilifu. Inawezekana, baadhi ya wazazi wetu sio wakamilifu. Yoashi alikuwa na familia isiyo ya wakamilifu akiwemo mpendwa wake (bibi) aliyeua kaka zake, ambaye pia angempata angemuua. Ukibaki kulaumu wazazi au watangulizi wako, unalaumu ukuu wa Mungu, haujileti kwake kwa msaada. Uchungu huo utakuumiza na wengineo wote na kukufanya ukose baraka za Bwana. Kuwa na mtazamo chanya ukue kiroho, na siyo kuridhika na "upendeleo kiroho" ulioupata.
2.Yoashi alionesha kuwajibika kiroho.
Yoashi aliwaelekeza makuhani kurejesha hekalu. Hatujui suala hili la hekalu lilichukua muda gani, lakini katika mwaka wake wa ishirini na tatu (1Fal 12:6 Yoashi alikuwa na miaka 30) mambo hayakuwa sawa, hivyo alimkabili Yehoyada (ambaye alikuwa ana umri unaokaribia miaka 120) ambaye labda kwa umri huu kazi ilimshinda. Makuhani walifanikisha kazi na ibada zikarejea (2Nya 24:14)
Jitihada hizi alizokuwa nazo Yoashi tunapashwa kuwa nazo sisi. Ujana ndio wakati wa kumtumikia BWANA kwa nguvu zote. Zaidi ya hapo, ujana ni lugha imetumika hapa, lakini kila aaminiye anahusika kumtumikia BWANA kwa nguvu zote.
3.Yoashi alipata jaribio kiroho;
Ukisoma 24:2 Yoashi alifanya jambo sahihi mbele za Mungu;
2 Mambo ya Nyakati 24:2
Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana siku zote za Yehoyada kuhani.Lakini baadaye Yehoyada kuhani alikufa wakati Yoashi akikumbana na jaribio kiroho;
2 Mambo ya Nyakati 24:17
Hata baada ya kufa kwake Yehoyada, wakuu wa Yuda wakamwendea mfalme, wakamsujudia. Naye mfalme akawasikiliza maneno yao.Mwovu pia huwa anao muda wake wa kujaribu mtu. Yehoyada alipokuwa hai, Yoashi hakujaribiwa, lakini alipokufa, jaribu likaja. Jaribu kwa Yoashi lilikuwa kawaida. Kwa kurejea, Musa aliwaonya Israeli kutorudia njia zao za awali baada ya kifo chake;
Kumbukumbu la Torati 31:29
Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa Bwana kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu.Ni muhimu kusimama kwa nafasi yako, maana huwezi kujua lini saa ya kujaribiwa kwako. Iko hatari ya kumkosea Mungu kwa kujaribiwa, ama kwa kujua au kwa kutokujua.
4.Yoashi alipewa muda wa kutubu;
Angalia somo la leo (juu kabisa, soma 19-20) ambapo tuaona nafasi ya toba iliyotolewa. Kwa neema yake, Mungu hatuachi katika dhambio zetu na uasi. Anatupa wakati wa kutubu na kumrudia. Mungu hataki kifo cha mtu mwovu, bali wote wamrudie kabla ya kufa;
Ezekieli 33:11
Waambie, Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, sikufurahii kufa kwake mtu mwovu; bali aghairi mtu mwovu, na kuiacha njia yake mbaya, akaishi. Ghairini, ghairini, mkaache njia zenu mbaya; mbona mnataka kufa, Enyi nyumba ya Israeli?Jambo la ajabu Yoashi alitoa hazina hekaluni! Hapa amemwacha Bwana! Haitegemewi kijana mwenye nguvu vile na imani kufanya maamuzi mepesi kama hayo ya kumkosea Mungu! Ndivyo tulivyo. Tumemkosea Bwana Bwana, lakini hajachoka, anatuita kutubu na kumrudia.
5.Yoashi alivuna maumivu ya uasi kwa Mungu.
Tumeona mwanzoni ambavyo Yoashi alimkosea Mungu, na Mungu akamwacha na jeshi likamvamia
(24:20) Yoashi aliiacha sheria ya Mungu, watumishi wa Yoashi wakamuasi, Yoashi akauasi ujumbe wa Zakaria, watumishi wa Yoashi pia wakamuasi. (24:21-25) Yoashi alimuua askari aliyejihami, watumishi wake wakamuua yeye, ukizingatia alikuwa mdhaifu. Yoashi hakuheshimu office ya unabii ya Zakaria, akampiga mawe. Yoshua alikufa kwa kuuawa na watumishi wake, akakosa heshima ya kuzikwa kwenye makaburi ya wafalme.Ujumbe wangu leo naweza kusema hivi;
"Matendo yako yataambatana na wewe".
Naongezea nukuu ya Mtume Paulo;
Wagalatia 6:7
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.Mwisho;
Nilitangulia kusema hivi; Upendeleo wa kiroho huhitaji uhalisia wa kiroho, vinginevyo itakuwa kusumbuka kiroho". Mungu amekupa nafasi ya kusikia neno lake. Unatembea katika uhalisia wa neno lake? Neno lake limekusaidia kupata msamaha wa dhambi? Anakutafuta urudi, ili usiwe mkristo mzuri aliyemaliza vibaya kama Yoashi, bali mkristo mzuri aliyekuwa shahidi wa Kristo hata hata mwisho akamaliza vizuri pia, kwa utukufu wa Mungu. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya