Date:
26-12-2024
Reading:
Matendo 12:1-4
Hii ni Noeli
Alhamisi tarehe 26.12.2024
Siku ya kukumbuka wafia dini
Masomo;
Zab 18:18-24
Mt 10:16-19
*Mdo 12:1-4
Matendo ya Mitume 12:1-4
1 Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa.
2 Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga.
3 Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa.
4 Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.
Uwe shahidi mwaminifu wa Kristo hata kufa;
Leo tunasoma juu ya Herode aliyewatenda vibaya watenda kazi wa Mungu. Wako Herode wengi, lakini tunayemsoma hapa leo ni Herode Agripa, hujulikana kama Herode Agrippa I (mjukuu wa Herode mkuu) aliyeishi 11KK hadi 44BK. Alikuwa mfalme wa Uyahudi 41 hadi 44KK. Huyu aliwatesa watumishi wa Mungu kama tulivyosema hapo juu. Somo linaonesha akimuua Yakobo, ndugu yake Yohana! Inawezekana aliwaua wengi, na labda huyo ndiye ameandikwa!
Baada ya kufanya hayo mauaji, akaona imewapendeza Wayahudi. Kumbuka alitesa na kuua watu waliohubiri Injili, ambapo baadhi ya Wayahudi walikasirika kusikia habari za Yesu zikihubiriwa, hivyo kukasirika kusingekosekana. Sasa katika kuwapendeza Wayahudi zaidi, akamkamata na Petro akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne wamlinde. Alitaka kumtoa baada ya Pasaka kumpeleka mbele ya watu!
Ukiendelea kusoma (6-19) unaona Petro akitolewa gerezani na malaika usiku. Tukio lilikuwa la kutisha hadi askari wakaogopa. Yupo ambaye alibatizwa usiku huohuo yeye na familia yake. Baadaye kuanzia mstari wa 20 unaona Herode akitoa hotuba katika kiti cha kifalme, hotuba ambayo haikumpa Mungu utukufu. Herode anapigwa na Mungu na kufa usiku huo huo.
Uwe shahidi mwaminifu wa Kristo hata kufa;
Tunaalikwa kuwa mashahidi waaminifu kama Petro aliyekuwa shahidi hadi gerezani akaja kuokolewa na malaika wa Bwana katikati ya usiku mnene. Uaminifu wake kwa Bwana ulimuokoa gerezani ili aendelee na utume wake. Lakini pia tuwe wema kwa watu wote, tusiwe kama Herode aliyelitesa Kanisa, tutaishia kuzimu kama Herode alivyoliwa na chango akafa. Hakuna shahidi mwaminifu anayetesa watu, mwongo, katili, mwizi, mzinzi n.k acha!
Kuwa shahidi mwaminifu wa Kristo hata kufa. Amina.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650