Hii ni Advent
Ijumaa asubuhi tarehe 20.12.2024
Ezekieli 18:26-32
26 Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa.
27 Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai.
28 Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.
29 Lakini nyumba ya Israeli husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, je! Njia zangu sizo zilizo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa?
30 Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu.
31 Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli?
32 Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.
Tubuni na kuiamini Injili;
Ezekieli analeta ujumbe kwa Taifa la Mungu kuhusu haki ya Mungu kwamba aendaye katika haki ya Mungu, halafu akaiacha hiyo njia ya haki, atakufa katika uovu wake. Naye mwovu akiuacha uovu wake ataiponya roho yake. Bwana anasema atawahukumu Israeli kwa kadri ya njia zake, hivyo anawaita kurudi kwake. Anawaita kuacha makosa yao na kutubu maana hafurahii watu wake kufa dhambini.
Hata leo Mungu wetu hafurahii watu wake kufa wakiwa dhambini. Anatutaka kutubu na kuiamini Injili ili tufe katika yeye. Somo linaonekana kutoa ujumbe kwa watu wa Israeli. Baada ujio wa Kristo, Israeli ni wote wamwaminio Yesu Kristo na kumpokea kama Bwana wao. Hivyo ujumbe huu ni wetu sote, kwamba tutubu na kuiamini Injili, Yesu anakuja. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa
Mlutheri