Hii ni Advent
Jumanne asubuhi tarehe 10.12.2024
Isaya 60:7-10
7 Makundi yote ya Kedari yatakusanyika kwako, Kondoo waume wa Nebayothi watakutumikia; Watapanda juu ya madhabahu yangu kwa kibali, Nami nitaitukuza nyumba ya utukufu wangu.
8 Ni nani hawa warukao kama wingu, Na kama njiwa waendao madirishani kwao?
9 Hakika yake visiwa vitaningojea, Na merikebu za Tarshishi kwanza, Ili kuleta wana wako kutoka mbali, Na fedha yao na dhahabu yao pamoja nao, Kwa ajili ya jina la Bwana, Mungu wako, Kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli, Kwa kuwa amekutukuza wewe.
10 Na wageni watajenga kuta zako, Na wafalme wao watakuhudumu; Maana katika ghadhabu yangu nalikupiga, Lakini katika upendeleo wangu nimekurehemu.
Ukombozi wetu umekaribia;
Huu ni ujumbe kwa Taifa la Mungu lililokuwa limetawanyika. Bwana anaonesha rehema yake kwa Taifa lake ambalo alilikusanya na kuliweka pamoja tena kwenye nchi yao. Somo linaonesha Bwana kuwatoa mbali, yaani kutoka nchi isiyokuwa kwao kwa ajili ya jina lake kama Bwana asiyewaacha watu wake.
Ujumbe wa Bwana unamalizika kwa kuonesha rehema ya Mungu (10). Huu ndiyo ujumbe wangu kwako asubuhi hii. Mungu anayo rehema kwa wote. Tuishi maisha ya imani ya kweli, toba na msamaha ili arudipo mara ya pili asituache. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa
Mlutheri