Ijumaa asubuhi tarehe 27.09.2024
Kumbukumbu la Torati 30:1-10
1 Tena itakuwa, mambo haya yote yatakapokujilia, baraka na laana nilizoweka mbele yako, nawe utakapozikumbuka kati ya mataifa yote, huko atakakokupeleka Bwana, Mungu wako,
2 nawe utakapomrudia Bwana, Mungu wako, na kuitii sauti yake, mfano wa yote nikuagizayo leo, wewe na wanao, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote;
3 ndipo Bwana, Mungu wako, atakapougeuza utumwa wako, naye atakuhurumia, tena atarejea na kukukusanya kutoka mataifa yote, huko alikokutawanyia Bwana, Mungu wako.
4 Watu wako waliotawanyika wakiwako katika ncha za mbingu za mwisho, kutoka huko atakukusanya Bwana, Mungu wako; kutoka huko atakutwaa;
5 atakuleta Bwana, Mungu wako, uingie nchi waliyomiliki baba zako, nawe utaimiliki; naye atakutendea mema, na kukufanya uwe watu wengi kuliko baba zako.
6 Bwana, Mungu wako, atautahiri moyo wako, na moyo wa uzao wako, ili umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai.
7 Na laana hizi zote Bwana, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa.
8 Nawe utarudi, uitii sauti ya Bwana, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo.
9 Na Bwana, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng'ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa Bwana atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako;
10 ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.
Uchaguzi wako ndiyo maisha yako;
Mungu anawaelekeza Israeli kumfuata, na anawawekea laana mbele yao ikiwa hawatamwamini na kumfuata, lakini anawawekea baraka mbele yao ikiwa watamwamini na kumfuata.
Bwana anaahidi kuwatoa Israeli katika utumwa iwapo watamfuata. Anaahidi kuwakusanya wakae pamoja katika yeye. Kubwa kuliko yote anawaita kuishika torati.
Sisi tuko huru, Kristo ametuokoa na sheria. Wokovu wetu hauna vitisho, ndiyo maana sisi hatuna habari za laana. Tunayo habari njema ya kuokolewa kwa neema kwa njia ya kifo cha Yesu msalabani. Ahadi inayodumu kwetu ni Imani katika Yesu Kristo ili tuwe na mwisho mwema. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa