Date:
11-09-2024
Reading:
Luka 21:1-4
Jumatano asubuhi 11.09.2021
Luka 21:1-4
[1]Akainua macho yake akawaona matajiri wakitia sadaka zao katika sanduku la hazina.
[2]Akamwona mjane mmoja maskini akitia mle senti mbili.
[3]Akasema, Hakika nawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote;
[4]maana, hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi, bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo.
Uwakili wetu kwa Bwana;
Yesu anaiongelea sadaka ya mjane kuwa timilifu maana katika umaskini wake alitoa vyote alivyokuwa navyo, kwa moyo wa shukrani. Matajiri walitoa mali iliyowazidi. Ingekuwa leo tungesema walitoa mabaki au"chenji".
Yesu alitaka kufundisha kuhusu kumtolea Mungu, kuwa sadaka isiwe kitu cha ziada, bali cha kwanza. Unapopata fedha/mali, wa kwanza kumpa ni Mungu, maana vyote ni mali yake.
Tunayo nafasi ya kujihoji, kuwa pamoja na baraka zote tulizopewa, tunamtolea Mungu inavyostahili au tunampa mabaki/chenji? Unaenda dukani kutafuta chenji kwa ajili ya sadaka, kwani kama siyo Mungu hiyo hela kubwa ungeipata? Moyo uliojaa shukrani hauwezi kumpa Mungu mabaki! Bali utampa vinono, yaani kumtolea inavyostahili.
Tukumbuke kuwa tunawajibika kumtolea Mungu kwa sababu sisi ni mawakili tu wa mali zake. Tunapomtolea tunampa mali yake. Lakini pia, matoleo yetu ni muhimu ili kazi yake iendelee. Unamtolea Mungu ipasavyo au unatoa chenji? Unamtolea kwa moyo wa shukrani? Siku njema. Amina.
Heri Buberwa