
Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front tarehe 20 Aprili 2025 ulijumuika na wakristo wote ulimwenguni kusherehekea Sikukuu ya Pasaka. Siku muhimu ya kukumbuka kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Somo: Yesu Mfufuka ni Tumaini la Wote Waaminio ~ Marko 16: 1-8
Akizungumza katika ibada ya kwanza iliyofanyika Usharikani hapa, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa alisema kuwa Pasaka ni sikukuu muhimu ambayo Yesu anawakomboa wanadamu kutoka katika vifungo vya shetani kupitia njia ya msalaba. “Kupitia njia hii ya msalaba Yesu anaturudishia uhusiano uliopotea kabisa kati yetu sisi wanadamu na Mungu aliyetuumba,” alisema.
“Kifo cha Yesu kilileta simanzi, kilileta huzuni, kilileta kutoamini kwa wengi waliokuwa wameanza kumwamini na hawakuwa ten ana ujasiri wa kupita mbele ya watu na kuliita jina la Yesu. Tangu alipokufa Yesu, saa tisa ile Ijumaa, wanafunzi wa Yesu tunaambiwa kuwa wwalienda kujifungia Galilaya na kujifungia kule hakukuwa kwa sababu nyingine yoyote bali ni kwa sababu ya aibu waliyokuwa nayo laikini wasikumbuke kuwa huyu Yesu aliahaidi kwamba siku ya tatu atafufuka. Lakini kujifungia kwao kule pia ilikuwa ni katika kuokoa maisha yao kwa sababu kukiri jina la Yesu hadharani ilikuwa ni hatari kwa kila mtu.
Hivyo furaha ya Kanisa kwa sikukuu hii ni kuthibitisha kwamba tunaye Mungu wa kweli ambaye anaishi, Mungu ambaye hatusherehekei kaburi lake bali tunasherehekea kufufuka kwake. Pasaka inaturuhusu kwa sababu hakuna mwingine katika ulimwengu huu ambaye aliwahi kufufuka wala atakayekuja kufufuka bali ni Yesu peke yake. Tunaye Mungu wa kweli, Mungu aliye hai, Mungu ambaye hayuko kaburini.” alisema Baba Askofu Malasusa.
Baba Askofu Malasusa pia aliwakumbusha washarika kutoogopa au kukaa kimya kwani Yesu alishinda umauti wa ajili yao na kwamba inabidi wawe na imani thabiti na kumtegemea Mungu katika kila jambo. “Asingefufuka Yesu Kristo, Imani yetu ingekuwa bure. Ziko imani nyingi katika ulimwengu huu, lakini wale walioanzisha imani hizo au waliozihubiri imani hizo, wao wenyewe walikufa. Yesu alikufa lakini akafufuka.”
Katika hatua nyingine Baba Askofu Malasusa aliwaasa washarika kutosherehekea sikukuu ya Pasaka kama desturi au kwa sababu ipo kwenye kalenda. Aliwataka kuhakikisha sikukuu hiyo inagusa maisha yao na kuwaokoa katika dhambi. “Hatuna haja ya kusherehekea Pasaka ambayo haigusi mioyo yetu na maisha yetu ya kiimani. Leo Yesu Kristo amefufuka, afufuke na maisha yetu,” alisema Baba Askofu Malasusa.
Baadhi ya Matukio katika Picha kutoka kwenye Ibada za Sikukuu ya Pasaka.
Tazama ibada za Pasaka hapa;
1. Ibada ya Kwanza (Kiswahili): https://www.youtube.com/watch?v=-1d6WiOgzuU
2. Ibada ya Pili ( English service): https://www.youtube.com/watch?v=eadHViyqaPE
3. Ibada ya Tatu ( Kiswahili): https://www.youtube.com/watch?v=rY-yyadA6wo
4. Ibada ya Jumatatu ya Pasaka (Kiswahili): https://www.youtube.com/watch?v=nNwYQTMn4Pg
-------------######----------------