Date: 
15-04-2025
Reading: 
1Petro 6:1-4

Hii ni Kwaresma 

Jumanne asubuhi tarehe 15.04.2025

1 Petro 4:1-6

1 Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi.

2 Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.

3 Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali;

4 mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.

5 Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.

6 Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai.

Tumshangilie Bwana;

Asubuhi ya leo, Petro anatuita kuwa mawakili wema wa neema ya Mungu pale anapotusihi kuwa na nia ya Kristo katika maisha yetu. Anatutaka tusiishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu. Petro anaendelea kusema kuwa wakati uliopita wa kutenda uovu umepita, ni muda sasa wa kuuacha huo uovu, yaani ibada ya sanamu. Mkazo wa Petro ni kuishi maisha ya imani maana kila mmoja atatoa hesabu kwa Mungu siku ya hukumu.

Petro anaelezea neema ya Mungu na hatma ya waaminio, kwamba ni Kristo pekee astahiliye kuaminiwa na kuabudiwa. Ndiye atakayewapa wamwaminio uzima wa milele. Tunapokumbuka Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe, tukumbuke kuwa alikuwa anaiendea njia ya mateso kuokoa ulimwengu, hivyo tudumu katika yeye ili tuwe na mwisho mwema. Amina

Jumanne njema

Heri Buberwa