Event Date: 
14-06-2023

Tarehe 14-15/06/2023 ilifanyika kambi ya watoto wa Shule ya Jumapili au Sunday School katika Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front Cathedral, ambapo ilifuatiwa na ziara ya watoto hao kutembelea Usharika wa Kitunda ambako pia waliungana na watoto wenzao kujifunza neno la Mungu.

Miongoni mwa mada zilizofundishwa kwa watoto hao ni pamoja na;

  • Afya, mazingira na ukuaji
  • Haki na wajibu wa watoto
  • Kufahamu na kupinga ukatili
  • Upendo na msamaha
  • Watoto na utandawazi

Akifungua kambi hiyo Mchungaji Joseph Mlaki aliwaasa walimu kuwapa mafundisho watoto ambayo yatawasaidia katika kuwajenga kimwili na kiroho. “Naomba mshike yote yale mtakayofundishwa hapa ili yaweze kuwasaidia namna ya kuishi na marafiki zenu na muwe mfaano wa watoto wengine,” alisema Mchungaji Mlaki.

Mchungaji Mlaki pia aliwashukuru wazazi na walezi kwa kufanikisha kambi hiyo kwa kuwaleta watoto wao kanisani ili kuungana na wenzao.

Akitoa mrejesho kwa washarika; Mwenyekiti wa Kamati ya Afya Dkt. Samuel Swai aliwashukuru wazazi na walezi kwa kujitoa kuwaleta watoto wao kanisani kujifunza. Alisema kwa siku zote mbili, zaidi ya watoto 200 waliweza kuhudhuria.

Pia Mchungaji Kiongozi wa Usharika, Chaplain Charles Mzinga pia alitoa shukrani za dhati kwa walimu, wazazi, walezi na wote waliofanikisha kambi ya watoto kufanyika katika Usharika wa Azania Front Cathedral. Chaplain Mzinga aliwaasa washarika kuendelea kutoa ushirikiano wa aina hiyo pindi fursa za kambi au semina zinapotangwazwa kwa makundi mbalimbali ikiwemo watoto.

Baadhi ya Picha kutoka kwenye kambi ya Watoto AZF

Kutazama baadhi ya matukio kutoka kwenye kambi ya watoto: https://www.youtube.com/watch?v=myJi0-2ng7Q&t=2160s