Date: 
18-05-2023
Reading: 
Luka 24:50-53

Alhamisi ya tarehe 18.05.2023

Siku ya kukumbuka kupaa kwa Bwana (Quadragesima)

Masomo;

Zab 110:1-7;

Ebr 6:17-20;

*Lk 24:50-53

Luka 24:50-53

50 Akawaongoza mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki.

51 Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao; akachukuliwa juu mbinguni.

52 Wakamwabudu; kisha wakarudi Yerusalemu wenye furaha kuu.

53 Nao walikuwa daima ndani ya hekalu, wakimsifu Mungu.

Yesu Kristo amepaa katika Utukufu wake;

Kuagana ambako ni kwa mara ya mwisho huwa ni kugumu, yaani "Kwa heri" ambayo wahusika wanapeana wakijua ni ya mwisho huwa ni ngumu. Lakini kwa maana ya Imani yetu, kwa heri ya mwisho huwa siyo ngumu, wala haitakiwi kuwa ya huzuni. Kwa sababu hii, hata wanafunzi hawakushtuka wala kushangaa Yesu alipopaa, bali walimwabudu na kurudi Yerusalemu wakiwa wenye furaha kuu.

Luka anaanza Injili yake akiwatangazia wachungaji kuhusu kuzaliwa kwa Yesu;

Luka 2:10-11

[10]Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote;
[11]maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

Sasa hapa mwishoni Luka anawaacha wasomaji wake kufikiri "kwa nini wanafunzi walijawa na furaha Yesu alipopaa?" Anataka tujitafakari, kama maisha yetu yamejawa na furaha kwa sababu Yesu amepaa.

Kumtafakari Yesu akipaa kutufanye tumwabudu na kufurahi. Kufufuka na kupaa kwa Yesu ni matukio mawili ambayo hayakutokea siku moja kama baadhi ya wasioamini wanavyodai. Kama tungelikuwa na kitabu cha Luka 24 peke yake, tungefikiri hivyo. Lakini katika kitabu cha Matendo ya Mitume 1:3-11, Luka anaeleza vizuri kuwa tukio hili la kupaa lilitokea baada ya siku 40 za ufufuko. Hapa nyakati hazikutofautiana sana. Kwa hiyo Yesu alifufuka, na baadaye alipaa. 

Mambo yafuatayo yanaweza kutuongoza katika kumwabudu na kufurahi;

1. Kupaa kwa Yesu kuliashiria kuhitimisha huduma yake duniani.

Yesu hakuondoka duniani kwa sababu ya kukataliwa na kusulibishwa na watenda dhambi. Hakupaa kwa sababu ya kukata tamaa. Aliondoka kwa sababu alimaliza kazi iliyomleta, yaani aliyotumwa na Baba. (17:4), na alisema pia;

Yohana 16:28

[28]Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba.

Alikuja kufanya nini?

Hatuna haja ya kuzunguka;

Mathayo 1:21

[21]Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.

Yesu ndiye Mungu kweli, alifanyika mwanadamu kwa ajili ya wokovu wetu. Kupaa kwake mbinguni kunaonyesha kumaliza kazi yake, na hilo litujaze ibada na furaha. Luka anasema wanafunzi walianza kumwabudu Yesu. Kama Yesu alifufuka, akapaa, na kama wanafunzi walivyomshuhudia, nasi hatuna budi kuungana nao kwa ibada, tafakari na furaha. Maana yake dhambi zetu zimeondolewa kwa jina lake. Tunafurahia upatanisho na Mungu kwa njia ya damu yake. Tuna uhakika na maisha yajayo, maana Yesu ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba, akisubiri siku ya kurudi kulichukua Kanisa. Hivyo tunayo haja ya kumwabudu na kufurahi, maana kazi yake imeisha.

2. Kupaa kwa Yesu kuliashiria kuanza kuanza kwa huduma yake mbinguni.

Yesu aliwaambia wanafunzi;

Yohana 14:28

[28]Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.

Hapa Yesu alionyesha nafasi yake kama Mwokozi, kwamba sio mwanadamu tu kama alivyoonekana. Yesu mwenyewe alionyesha kumtegemea Baba. Pamoja na utukufu wake kudharauliwa, Yesu alijiweka mikononi mwa Baba yake akiomba mapenzi yatimizwe. Lakini Utukufu wake uko pale pale, na atarudi kulichukua Kanisa. Aliahidi na akamtuma Roho Mtakatifu kwa wanafunzi ili awaimarishe katika maisha na huduma yao kwa ujumla.

Huduma ya Yesu mbinguni ina mambo yafuatayo;

-Kuanzisha huduma ya kuliombea Kanisa

-Kuandaa makao ya watu wake

-Kwamba Yesu yupo, leo na hata milele, mbinguni na duniani.

-Uvuvio wa Roho Mtakatifu. 

3. Kupaa kwa Yesu kuliashiria kuanza kwa huduma yetu kama wawakilishi wake hapa duniani.

Yesu hakupaa na wanafunzi wake, kwa sababu alikuwa na wajibu aliowaachia waufanye katika jina lake. Kazi yao, kazi yetu leo, ni kuhubiri toba na msamaha wa dhambi tukijawa na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Kwa huduma yetu, tuzingatie yafuatayo;

-Yatupasa tuwe na baraka zake katika maisha na huduma yetu kwa ujumla kama Yesu alivyotubariki.

-Tumwabudu kabla na baada ya kazi yake. Yaani tumwabudu wakati wote.

-Tuwe na furaha katika huduma yetu.

Wanafunzi walienda zaidi ya siku 40 za kuwa pamoja na Kristo mfufuka wakitafakari katika kupaa kwa mtazamo mpya kwa Utukufu wa Mungu. Waumini wote wa kweli wana uelewa wa kuuona Utukufu wa Mungu katika Kristo Yesu. Tunapouona Utukufu wa Mungu kwa Yesu aliyefufuka na kupaa, tujazwe ibada, furaha na shukrani kwa Mungu, kwa ajili ya rehema. Kama bado unakosa vitu hivi, omba Yesu atimize haja ya moyo wako. Mtafute yeye bila kuchoka. 

Kwa macho yetu, kupaa kunaonekana kama hali ya mtu kukwea juu mawinguni, lakini kwa mtazamo wa kiMungu, kupaa ni Yesu anaporudi nyumbani kwa Utukufu.

Mwisho;

Kama tunavyokiri katika Ukiri wa Imani;

"...Siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu, akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Mungu Baba mwenyezi, kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu....." Tuadhimishe na kukumbuka kupaa kwa Yesu, tukijua kuwa Yesu atarudi tena.

Hivyo unawajibika kujiandaa ili Yesu akirudi usiachwe.

Nakutakia ibada njema ya kupaa kwa Yesu Kristo.

 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com