Mchungaji Charles Mzinga akipokea mavuno katika mtaa wa Tabora.
Mtaa wa Tabora ni mmojawapo kati ya mitaa mitano inayotunzwa na Usharika wa Kanisa Kuu la Azaniafront Cathedral. Mtaa huo unapatikana katika wilaya ya Mkulanga mkoani Pwani ukiwa na washarika takribani 120.
Miongoni mwa huduma za kichungaji zitolewazo kwenye mitaa inayotunzwa na Usharika wa Kanisa Kuu ni pamoja na kufungisha ndoa, ubatizo, ushiriki wa meza ya Bwana, kipaimara, kupokea wakristo wageni wanaotoka katika madhehebu mengine, kurudisha washarika kundini na kuhudumu katika sherehe mbalimbali zilizo katika kalenda ya kanisa.
Jumapili ya tarehe 20 Septemba 2020, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchg Charles Mzinga alifanya ziara ya huduma katika mtaa wa Tabora. Huduma zilizotolewa siku hiyo ni pamoja na ubatizo wa watoto wawili, kipaimara kwa vijana wawili pamoja na washarika wa mtaa huo kupata fursa ya kushiriki meza ya Bwana.
Pia katika ibada hiyo, Mchungaji Mzinga alipokea mavuno ya washarika wa mtaa huo ambao wengi wao wanajipatia kipato kupitia shughuli za kilimo pamoja na ufugaji. Aidha, mtaa huo kwa sasa uko chini ya usimamizi wa Mwinjilisti Onesmo Uroki.
Akizungumza katika ibada takatifu ilyofanyika mtaani hapo, Mchungaji Mzinga aliwapongeza washarika kwa kuendelea kujitokeza kanisani kumwabudu Mungu mbali na changamoto mbalimbali wanazozipitia. “Natambua kuwa wengi wa washarika hapa wanatoka umbali mrefu kuja kujumuika na wenzenu kumtukuza Muumba wetu. Huo ndio ukristo, hakuna kukata tamaa. Pia niwapongeze wote kwa kutoa mavuno yenu ya mwaka huu. Ni matumaini yangu kuwa mwakani mavuno mashambani mwetu yataongezeka maradufu”, alisema Mchungaji Mzinga.
Katika ziara hiyo, Mchungaji Mzinga aliambatana na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wazee la Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uinjilisti, Mzee Simon Jengo. Baada ya Ibada, Mchungaji Mzinga pamoja ujumbe wake walipata kushiriki chakula cha mchana pamoja na washarika wa mtaa huo.
Ziara za kutembelea, kukagua maendeleo pamoja na kutoa huduma za kichungaji katika mitaa inayotunzwa na Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront zimerejea tena mnamo mwezi Septemba mwaka huu baada ya kusimama kwa miezi kadhaa kutokana na janga la Covid-19. Kabla ya ziara hii, tarehe 6 Septemba 2020, Mchungaji Mzinga alitembelea mtaa mwingine wa Viwege unaopatikana katika maeneo ya Chanika jijini Dar es Salaam.