Hii ni Epifania
Alhamisi asubuhi tarehe 08.01.2026
1 Wafalme 19:11-14
11 Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi;
12 na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu.
13 Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya?
14 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe.
Yesu ni nuru ya Ulimwengu;
Baada ya Eliya kuwashinda manabii wa Baali, Eliya alikuwa amejificha. Akiwa amejificha Bwana akamtokea. Soma alivyomtokea na kilichoongelewa;
1 Wafalme 19:9-10
9 Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? 10 Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.Somo la asubuhi hii linaanzia hapo (soma tena). Bwana anamwambia Eliya kutoka alipojificha. Ukatokea upepo mkubwa, likafuatia tetemeko la nchi, baadaye ukatokea moto, na baadaye sauti ndogo ya utulivu. Eliya akaitwa tena na Bwana. Akasema anaona wivu kwa ajili ya Bwana, kwa kuwa wana wa Israeli walikuwa wameyaacha maagano ya Bwana, na walikuwa wakimtafuta wamuue!
Ukiendelea kusoma unaona Bwana akimtuma Eliya kwenda kuwapaka mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu, Yehu awe mfalme wa Israeli na Elisha kuwa nabii. Huu ulikuwa mpango wa Mungu kuwakomboa watu wake, hakuwaacha japo walikuwa wamemuasi. Ndiyo ahadi ya Mungu kwetu, kwamba hatuachi daima. Ahadi hii utimilifu wake ni Yesu Kristo aliye nuru ya Ulimwengu, ambaye tukimwamini na kumfuata tutaurithi uzima wa milele. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa
