Hii ni Advent
Jumatano asubuhi tarehe 18.12.2024
Isaya 61:1-5
1 Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.
2 Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao;
3 kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.
4 Nao watajenga mahali pa kale palipoharibiwa, watapainua mahali palipokuwa ukiwa zamani, watatengeneza miji iliyoharibiwa, mahali palipoachwa kizazi baada ya kizazi.
5 Na wageni watasimama na kulisha makundi yenu, na watu wa kabila nyingine watakuwa wakulima wenu, na watunzaji wa mizabibu yenu.
Tubuni na kuiamini Injili;
Isaya alitabiri habari njema ya ukombozi kwa ulimwengu, akitangaza wokovu kwa wote. Katika ukamilifu wa utabiri huo, Yesu alikuja duniani akileta habari njema ya wokovu kama ilivyotabiriwa.
Kwa kuonesha utabiri huu kukamilika, Yesu alisoma neno hili hekaluni;
Luka 4:17-19
17 Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, 18 Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, 19 Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.Yesu alikuwa akikazia unabii kutimia, kwamba yeye ndiye alitoka mbinguni kuleta wokovu. Hivyo tunawajibika kusafisha mioyo yetu ili huyu Yesu aliyeleta wokovu aingie na kukaa kwetu, sasa na hata milele. Amina
Jumatano njema.
Heri Buberwa