Jumanne asubuhi tarehe 30.07.2024
Waamuzi 2:1-5
1 Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;
2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?
3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.
4 Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia.
5 Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia Bwana sadaka huko.
-
Mungu hupendezwa na mwenye moyo wa toba;
Wana wa Israel baada ya kufika Kanani, walianza kuweka maagano na wenyeji waliowakuta. Walishirikiana nao hadi kwenye madhabahu zao. Jambo hili halikumpendeza Bwana, ndiyo maana somo linaonesha malaika wa Bwana akiwapelekea ujumbe kuhusu jambo hilo. Baada ya ujumbe huo kutoka kwa Bwana, tunaona Israel wakimlilia Mungu na kumtolea sadaka ili awasamehe.
Israeli walipewa ujumbe kwamba walikosea, wakatubu. Sisi nasi ni wenye dhambi, hakuna asiye na dhambi kama neno la Mungu linavyosema;
1 Yohana 1:8-10
8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. 9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. 10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.Tunakumbushwa kufanya toba kila wakati ili Kristo atusamehe, akae ndani yetu daima na atupe uzima wa milele. Amina.
Jumanne njema
Heri Buberwa