Washarika wakinawa mikono kwa maji tiririka pamoja na sabuni maalum ili kuweka mikono yao safi kabla ya kuingia kanisani kwa ajili ya Ibada. Picha: AZF/Paulin Paul
Tangu mwezi Disemba mwaka 2019, dunia imekuwa katika hali ya taharuki ikijaribu kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19), ugonjwa ambao, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), ulianzia katika jimbSo la Wuhan nchini China kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya dunia ikiwemo nchini Tanzania.
Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na jumuiya ya kimataifa, taasisi binafsi pamoja na serikali za mataifa mbalimbali ili kupunguza au kutokomeza kabisa maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vimeonekana kuwa tishio kwa maisha ya binadamu kiasi cha WHO kuitangaza COVID -19 kama janga la ulimwengu.
Nchini Tanzania, Wizara ya Afya imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali kwa wananchi juu ya namna bora ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona pamoja na kutoa huduma stahiki kwa ambao wamethibitika kukutwa na virusi hivyo baada ya kufanyiwa vipimo.
Shughuli mbalimbali za kibinadamu (kijamii na kiuchumi) zimeweza kuathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kusambaa kwa virusi vya Corona. Kwa mujibu wa WHO, tahadhari ya kwanza ya kukabiliana na kusambaa kwa kasi kwa virusi hivyo ni kupunguza misongomano ya watu pamoja na kunawa mikono mara kwa mara kwa kutumia dawa maalumu za kuua vijidudu (sanitizer).
Kwa upande wa kanisa, Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront umekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za serikali za kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya Corona kwa kutoa elimu juu ya namna bora ya kujikinga kwa washarika kila siku za Jumapili katika ibada zote. Pia usharika uliweka vifaa maalumu vya kunawa mikono katika kila mlango wa kuingia kanisani pamoja na ofisi za usharika ili watu wote wanaoingia na kutoka katika mazingira ya kanisa weweze kujikinga.
Usharika, kwa kushrikiiana na Dayosisi ya Mashariki na Pwani pia umelazimika kubadili baadhi ya taratibu za ibada ikiwa ni pamoja na washarika kupungiana mikono badala ya kusalimiana kwa kugusana, kupunguza mazoezi ya kwaya kutoka mara mbili kwenda mara moja kwa wiki, kusitisha ibada za jumuiya (nyumba kwa nyumba) na kusitisha madarasa yote ya kipaimara kwa muda usiojulikana. Pia ibada ya wazee iliyokuwa imepangwa kufanyika tarehe 4 Aprili 2020 sasa imehairishwa mpaka tarehe nyingine itakapotangazwa.
Akizungumza katika ibada ya siku ya Jumapili tarehe 22 Aprili 2020 juu ya janga la Corona linaloikabili dunia kwa wakati huu, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azaniafront, Mchungaji Charles Mzinga aliwataka washarika kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya ili kujikinga na COVID-19.
Aidha, Mchungaji Mzinga aliwataka washarika kuendelea kujitokeza kanisani ili kumwomba Mungu licha ya hofu iliyotanda mitaani juu ya maambukizi ya virusi vya Corona. “Napenda nitoe wito kwa washarika kujitokeza kanisani kumwomba Mungu ili atunusuru na janga hili huku tukichukua tahadhari zote zinazotolewa na mamlaka husika”, alisema Mchungaji Mzinga huku akiongeza kwamba, usharika utandelea kutoa taarifa za mara kwa mara kwa washarika wote juu ya mwenendo wa suala hili, “Kama kutakuwa na mabadiliko mengine yoyote juu namna ya uendeshaji wa shughuli zetu za kila siku hapa usharikani, tutawafahamisha washarika wote haraka iwezekanavyo”.
Kupata takwimu na taarifa mbalimbali za kina juu ya virusi vya Corona kwa ulimwengu mzima tembelea; https://www.who.int/emergencies/diseases/novel-coronavirus-2019