Date: 
14-07-2022
Reading: 
1 Wafalme 3:16-24

Alhamisi asubuhi tarehe 14.07.2022

1 Wafalme 3:16-24

[16]Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.

[17]Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.

[18]Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.

[19]Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia.

[20]Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.

[21]Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa.

[22]Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.

[23]Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.

[24]Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.

Mungu ni mwingi wa huruma na haki;

Suleimani aliomba hekima kwa Mungu ili aweze kuongoza Taifa lake. Pale wanawake wawili walipogombania mtoto mbele yake akaamuru upanga uletwe. Ukiendelea kusoma mstari wa 25, unaona mzazi mmoja akiomba mtoto asikatwe apewe mwenzake. Na mwingine anaomba akatwe, wagawane marehemu! Suleimani anaamuru apewe yule aliyesema asikatwe.

Leo sitamuongelea Suleimani. Naongelea hawa wanawake wawili. Bila shaka aliyeomba mtoto akatwe hakuwa mzazi halisi! Ndiyo maana hakumwonea huruma mtoto aliyeishi. Alitaka afe kama wa kwake, na mwenzake apoteze mtoto kama yeye. Aliye mzazi halisi ndiye aliomba mtoto asikatwe.

Mzazi halisi hawezi kukubali mtoto wake afe. Huruma ya Mungu kwetu inazidi ya mzazi juu ya mtoto. Ndiyo maana Yesu aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Alipigwa yeye, alikufa yeye, tuliokombolewa ni sisi. Hii ndiyo huruma ya Mungu. Tunaitwa kudumu kwa Yesu mwenye huruma siku zote za maisha yetu.

Alhamisi njema.