Date:
10-01-2025
Reading:
Mithali 13:9
Hii ni Epifania
Ijumaa asubuhi tarehe 10.01.2025
Mithali 13:9
Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
Yesu ni nuru ya Ulimwengu;
Suleimani katika mstari huu tunaosoma asubuhi ya leo anaandika juu ya nuru ya mwenye haki kung'aa sana. Kwa wakati ule Suleimani anamtaja mtu aliyeishika sheria ya Bwana na kuitimiza torati yote kama mwenye haki. Huyu alionekana kutokuwa gizani, ndiyo maana anaandika kwamba nuru yake yang'aa sana. Asiyeshika sheria alionekana mbaya, hivyo taa yake kuzimika!
Ujumbe wa Suleimani unatutafakarisha juu ya imani katika Yesu Kristo, kwamba tukimwamini Yesu tunakuwa nuruni, kinyume chake tunakuwa gizani. Kwa maana ya tafakari katika zama za Agano jipya, mstari wa leo naweza kuuandika hivi;
"Nuru yake amwaminiye Kristo yang'aa sana; Bali taa ya asiyeamini itazimika".
Ujumbe wangu kwako asubuhi hii ni sisi sote kukaa nuruni, yaani kukaa katika Kristo ili tuufikie mwisho mwema tulioahidiwa katika yeye. Amina.
Ijumaa njema
Heri Buberwa