Jumatano ya tarehe 31.12.2025
Siku ya mwisho wa mwaka;
Masomo; Zab 65:7-13; Ebr 13:8
*Lk 17:11-19
Luka 17:11-19
11 Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.
12 Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,
13 wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!
14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika.
15 Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu;
16 akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.
17 Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?
18 Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?
19 Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.
Bwana ametutendea makuu;
Utangulizi;
Ukoma ulikuwa unatisha wakati wa Agano la kale na wakati wa Yesu. Kwa sehemu kubwa ni hali ambayo ilionekana kutokuwa na tiba na yeyote aliyeonekana kuwa mwenye ukoma hakutakiwa kuchanganyika na watu. Hii ni kwa sababu mtu mwenye ukoma alionekana kuwa najisi! Hii siyo dhana ya kufikirika, bali lilikuwa agizo tangu kale. Soma hapa chini kuangalia hilo agizo;
Mambo ya Walawi 13:45-46
45 Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi.
46 Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.
Katika Israeli watu wenye ukoma walitengwa, hadi ijulikane ukoma ulitokana na nini (Law 13:5). Mtu kuwa na ukoma alionekana asiye msafi! Kwa Myahudi kumgusa mwenye ukoma ilikuwa karibia sawa na kumgusa maiti! Baadaye waliruhusiwa kuingia kwenye sinagogi, ambapo walitakiwa kuwahi kuingia mapema kuliko wengine na kukaa sehemu yao maalumu ili wasichangamane na wengine wasio na ukoma. Walimu wa sheria waliamini kupona ukoma ilikuwa vigumu kama kumfufua aliyekufa. Katika historia ya Biblia, kabla ya somo la leo ni watu wawili tu waliokuwa wamepona ukoma. Wa kwanza ni Miriamu aliekuwa na ukoma kwa siku saba kama adhabu kwa kuwa kinyume na uongozi wa Musa (Hes 12:9-15) na Naamani Jemedari wa jeshi kutoka Dameski (2Fal 5) ambaye alipona ukoma baada ya kutii maelekezo ya Elisha na kuoga mtoni mara saba. Inakadiriwa kwamba hadi tukio la somo leo linatokea, alikuwa hajapona mtu ukoma kwa takribani miaka 700.
Somo lenyewe;
Nimeweka utangulizi huo ili uone watu waliokuwa na ukoma walionekanaje, waliishije, waliingiaje hekaluni n.k. Ni watu walioishi maisha ya kutengwa. Yaani walitengwa na jamii, na hekaluni pia!! Fikiria mtu ambaye ana ukoma, hawezi kufanya kazi kwa ukamilifu kwa sababu ya hali yake, lakini katika jamii aliyomo haruhusiwi kuchanganyika na yeyote! Kwa maana hiyo inaonekana ilipowezekana walikaa kwa makundi. Ndiyo maana tunaona leo wakimwendea Yesu kwa pamoja. Pamoja na kumuona Yesu, bado waliheshimu kutengwa kwao, walimwona Yesu lakini walisimama mbali! (12) wakaomba rehema kwa Yesu. Walijiona wakosaji! Yesu akawaambia waende kwa makuhani na walipokuwa wakienda wakatakasika, yaani wakapona ukoma. Jambo la ajabu aliyerudi kushukuru ni mmoja. Wengine hawakurudi, ni furaha ikiwazidia? Binafsi nafikiri walisahau kumshukuru Mungu. Sasa somo hili linatufundisha nini?
1.Imani katika Yesu Kristo.
Siamini kama wale ndugu walimuona Yesu mara moja tu wakaomba rehema. Bila shaka walikuwa wamesikia habari zake, wakawa na imani katika yeye. Yesu mwenyewe anagusia imani pale anapomwambia yule aliyerudi kushukuru kwamba "...enenda zako, imani yako imekuokoa". Kumbe tunaokolewa kwa imani kwa njia ya Yesu Kristo. Basi tusiiache imani hii.
2.Wokovu ni kwa wote
Kama nilivyoeleza kwenye Utangulizi hapo juu, watu wenye ukoma walitengwa. Hawakutakiwa kuchangamana na watu. Walionekana tofauti wasiostahili kukaa katikati ya wengine. Yesu leo tunaona akiondoa kizuizi hicho. Hili ni tangazo mahususi kabisa leo, kwamba wokovu ni kwa wote. Wote tu wenye dhambi tunaostahili msamaha kwa neema ya Mungu. Sote tunaitwa kwenda kwa Yesu, asibaki hata mmoja.
3.Wokovu ni maisha halisi, siyo maigizo
Yesu aliwaambia walioponywa wakajioneshe kwa makuhani. Katika kitabu cha maombi na miujiza cha mwaka 2015, Askofu Dkt. Abednego Keshomshahara, Mchg. Dkt. Elmereck Kigembe na Mchg. Alex Kasisi wakiwa waandishi, wanasema Yesu alitaka waende kwa makuhani walikoabudu maana wao ndio waliowafahamu, wakatoe sadaka huko. Tofauti na leo, unaweza kukuta mkutano uko Tanganyika Packers, mhubiri katoka Arusha, aliyepona katoka Dodoma, hakuna anayemjua. Inakuwa rahisi kufanya utapeli kwa kukusanya sadaka. Kwa hiyo Injili ya kweli ni maisha halisi, tuache uongo na usanii.
4.Tuwe watu wa shukrani
Hapa ndipo kuna lengo la somo la leo, ibada ya mwisho wa mwaka. Kati ya walioponywa kumi alirudi mmoja kushukuru! Wakati waliponywa wote kumi! Hii haikuwa sawa. Sawa nasi leo tujihoji, tumemaliza mwaka salama tukiwa wazima. Pamoja na changamoto tulizopitia, lakini tunamaliza mwaka tukiwa wazima. Tunamshukuru Mungu inavyostahili? Wote? Tumshukuru Mungu siyo leo tu, bali siku zote.
Mungu ametutendea makuu;
Mungu aliwatendea makuu wakoma kumi wakatakasika, ila aliyerudi kushukuru ni mmoja. Waliobaki tisa hawakuyaona makuu ya Mungu? Naamini waliyaona lakini hawakurudi kushukuru. Sisi tumuige aliyerudi kushukuru. Tumshukuru Mungu aliyetuwezesha kumaliza mwaka wa 2025 ambalo ni tendo kuu, na tumuombe kwa neema yake atufikishe mwaka mpya wa 2026. Ombi langu kwako, kuwa mtu wa shukrani kwa Mungu daima. Amina
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
